Phone: +255 (0) 26 2960150 | Email: info@ntlp.go.tz
Home / Media / Blog / TATHIMINI YA UTEKELEZAJI WA MPANGO MKAKATI WA SITA WA MPANGO WA TAIFA WA KUTOKOMEZA KIFUA KIKUU NA UKOMA, 2020-2025 YAANZA KUFANYIKA

TATHIMINI YA UTEKELEZAJI WA MPANGO MKAKATI WA SITA WA MPANGO WA TAIFA WA KUTOKOMEZA KIFUA KIKUU NA UKOMA, 2020-2025 YAANZA KUFANYIKA

image

Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma kwa kushirikiana na wadau kutoka ndani na nje ya nchi wameanza rasmi kufanya zoezi la tathimini ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Sita wa kutokomeza magonjwa ya Kifua Kikuu na Ukoma wa (NSP VI 2020-2025).  Tathimini hii ambayo hufanyika kila baada ya miaka mitano ina lengo la kupima ufanisi wa utekelezaji wa mkakati huu ulioanza kutekelezwa mwaka 2020 hadi 2025. Zoezi hili limehusisha mahojiano ya viongozi na wadau mbalimbali walioshiriki katika ngazi mbali mbali za utekelezaji kuanzia tarehe 1 hadi 5 Septemba 2025.

Akizungumza na timu ya wataalamu, Dkt. Rashid Mfaume Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI alisema ushirikiano mzuri uliyopo kati ya Wizara ya Afya na OR-TAMISEMI na wadau katika utekelezaji wa afua za kutomekeza Kifua na Ukoma ngazi ya Mkoa na Halmashauri, Pamoja uwepo wa sera na usimamizi dhabiti umechangia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza kiwango cha maambukizo ya magonjwa haya nchini.

images-1.png

Kwa upande wake Bi. Adella Mpina, Mratibu wa Programu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (OWM) alisema kuanzia Mwaka 2023, OWM kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta wamekuwa wakitekeleza Mpango wa Uwajibikaji wa Kisekta wa Mapambano dhidi Kifua Kikuu wenye lengo la kuongeza rasilimali muhimu kutoka Wizara zote, Licha ya jitihada hizo bado kumekuwa na mwitiko mdogo kutoka sekta nyingine hivyo kuwepo kwa haja ya kuongeza utashi na uelewa kwa Wizara za Kisekta nchini.

Katika hatua nyingine Bw. Amour Amour, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Afya alisema kwa mwaka wa Fedha 2025-2026 Serikali imetenga kiasi cha Bilioni 141 Kwa ajili ya kusadia mapambano dhidi ya magonjwa ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria nchini sanjari na jitihada mahususi za Serikali ya Awamu ya Sita za kufikia malengo ya kutokomeza magonjwa hayo ifikapo 2030.

images-2.png

Aidha, Mtaalamu Mshauri kutoka Shirika la Kimataifa la KNCV Tuberculosis Foundation la nchini Uholanzi, Dkt. Demelash Assefa alipongeza kuwepo kwa uhusiano na ushirikiano  mzuri uliopo kati ya Wizara ya Afya, OR-TAMISEMI na Ofisi ya Waziri Mkuu katika uratibu wa afua za Kifua Kikuu na Ukoma pamoja na utekelezaji wa sera ya afya  katika ngazi ya afya ya msingi.

Kukamilika kwa tathimini hii jumuishi kunategemea kutoa mapendekezo ya kuandaa Mpango Mkakati Mpya wa Saba ya Kutokomeza Kifua Kikuu na Ukoma nchini utakaoanzia Mwaka 2026 hadi 2030.

images-3.png