Timu ya wataalamu wa zoezi la tathmini ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Taifa wa Sita wa kupambana na Kifua Kikuu na Ukoma imewasilisha taarifa fupi ya zoezi hilo katika Ofisi ya Shirika la Afya Duniani (WHO) leo Septemba 12, 2025 Jijini Dar es Salaam.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Mtaalamu Kiongozi Dkt. Jarene DeguĀ kutoka Shirika la KNCV Foundation la Uholanzi, alisema kwa ujumla zoezi hilo lilimeenda vizuri na hali ya mapambano ya kutokomeza Kifua Kikuu na Ukoma nchini inakwenda vizuri japo kumeonekana kuwepo kwa vikwazo vichache katika uibauji wa wagonjwa pamoja na mwitiko katika maeneo yenye makundi hatarishi ya Kifua Kikuu kama machimboni.
Aidha amepongeza jitihada za Serikali katika kukabiliana na upungufu wa rasimali kutoka kwa wadau wa nje, ikiwemo ongezeko la bajeti na mpango wa bima ya afya kwa wote.
Kwa upande mwingine, Dkt Fedjo Tefoyet Galbert kaimu Mwakilishi Mkazi wa Shirika hilo hapa nchini alionesha kuridhishwa na taarifa hiyo hasa katika maeneo ya uendelevu na ujumuishi wa utoaji huduma za afya kwa pamoja (Health Programs Integration mechanism) akisema kuwa Wadau na Serikali hawana budi kuwekeza katika dhana hiyo ili kufikia malengo ya kitaifa ya kutokomeza magonjwa hayo kwa kutumia rasimali chache zilizopo.
Aidha kwa niaba ya Meneja Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma Dkt Allan Tarimo, aliishukuru timu hiyo kwa kuongoza kikamilifu zoezi hilo na kuja na mapendekezo yenye manufaa kwa nchi, Pia aliongeza kwa kusema, kukamilika kwa awamu hii ya tathimini kuna fungua nafasi ya kuanza maandalizi ya Mkakati Mpya wa Saba wa Taifa kwa mwaka 2026 - 2030 sanjari na vipaumbele vya Sekta ya Afya yaani (HSSP VI) unaoandaliwa pia.