Phone: +255 (0) 26 2960150 | Email: info@ntlp.go.tz
Home / Media / Blog / WADAU WAKUTANA KUJADILI NA KUTHIBITISHA MPANGO MKAKATI WA SABA WA KUTOKOMEZA KIFUA KIKUU NA UKOMA NCHINI 2026 - 2031

WADAU WAKUTANA KUJADILI NA KUTHIBITISHA MPANGO MKAKATI WA SABA WA KUTOKOMEZA KIFUA KIKUU NA UKOMA NCHINI 2026 - 2031

image

Wadau wa kupambana na magonjwa ya Kifua Kikuu na Ukoma wamekutana tarehe 29 Januari, 2026 mjini Morogoro kujadili na kuthibitisha mpango mkakati wa Saba wa kupambana na Kifua Kikuu na Ukoma wa kuanzia mwaka 2026 hadi 2031.

Akifungua kikao kazi hicho Dkt. Samuel Lazaro Mkuu wa Programu Wizara ya Afya alisema uthibitisho wa nyaraka hii ni hatua muhimu na inapaswa kuzingatia vipaumbele tulivyonavyo vya kitaifa na kimataifa ili kufikia malengo ya nchi na Kidunia ya kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu na Ukoma ifikapo mwaka 2030.

images-1.png

Kwa upande wake Dkt Johnson Lyimo kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) ameeleza ya kwamba katika mchakato wa kuandaa Mkakati huu, WHO limeshiriki kikamilifu na Wizara ya Afya na afua zilipo zinakidhi miongozo ya kimataifa ya kutokomeza magonjwa hayo mawili.

Aidha, Dkt. Bhavin Jani Mratibu Diwati la Misaada ya Nje kutoka Ubalozi wa Marekani alisema wataendelea kushirikiana na Serikali katika kupambana na kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu nchini kwasababu ugonjwa huo ni miongoni mwa magonjwa ya kipaumbele.

Ndugu Simon Magembe Mchumi  kutoka Wizara ya Fedha alisisitiza kama nchi tunapaswa kujikita katika kutafuta na kutenga rasilimali za ndani kwa ajili ya kupambana na magonjwa ya Kifua Kikuu, UKIMWI na Malaria, hivyo mpango mkakati huu una wajibu wa kujikita  katika kutafuta rasilimali za ndani za kupambana na magonjwa haya nchini.

Akichangia katika mjadala Dkt. Leornard Subi Mkurugenzi wa Hospitali ya Magonjwa Ambukizi ya Kibong’oto alisema licha ya kuwepo kwa jitihada kubwa zilizofanywa na serikali katika kupambana na magonjwa haya bado kuna haja ya mkakati huu kuweka mipango madhubuti ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu magonjwa haya pamoja.

Aliongeza kwa kusema, uimarishwaji wa afua za mipakani za kupambana na Kifua Kikuu pamoja na kuweka mikakati katika majiji yenye misongamano mikubwa ya watu ni maneneo mengine ambayo yanahitaji ufuatiliwaji wa karibu ili kupunguza kasi ya maambukizi mapya nchini.

Kikao kazi hicho kimehudhuriwa na washiriki kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Wizara ya Afya, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Wazri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Wadau kutoka Diwati la Misaada ya Nje Ubalozi wa Marekani, WHO, CDC, AMREF, MKUTA, MKIKUTE CSSC pamoja na wadau wengine wa kupambana na Kifua Kikuu na Ukoma nchini.