Phone: +255 (0) 26 2960150 | Email: info@ntlp.go.tz
Home / Media / Blog / SERIKALI KUWEKA MIKAKATI MADHUBITI KUONGEZA KASI YA UIBUAJI WA WAGONJWA WA KIFUA KIKUU NA UKOMA

SERIKALI KUWEKA MIKAKATI MADHUBITI KUONGEZA KASI YA UIBUAJI WA WAGONJWA WA KIFUA KIKUU NA UKOMA

image

Serikali imeendelea kuimarisha mikakati ya kuongeza kasi ya uibuaji wa wagonjwa wa Kifua Kikuu (TB) na Ukoma nchini kwa kuimarisha uchunguzi wa makundi yaliyo katika hatari na watu wenye dalili za TB katika jamii na vituo vya kutolea huduma za afya.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mwenyekiti wa Waganga Wakuu wa Mikoa Dkt. Charles Rashid Mkombachepa, wakati wa kikao kazi kilichofanyika mkoani Morogoro kuanzia tarehe 13 hadi 15 Agosti 2026.

Dkt. Mkombachepa amewataka watoa huduma za afya na wadau katika ngazi za mikoa na wilaya kuimarisha ufuatiliaji wa watu waliokutana na wagonjwa wa TB, kutumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii katika uibuaji na utoaji wa rufaa, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma, binafsi na jamii. Hatua hizo zinalenga kuhakikisha watu wenye dalili za TB wanagunduliwa, kuchunguzwa na kupimwa mapema, na wanaobainika kuwa na TB waanzishiwe matibabu kwa wakati.

Aidha, alisisitiza matumizi ya takwimu katika kutambua maeneo yenye kiwango kikubwa cha maambukizi TB, kuimarisha kampeni za uelimishaji na uhamasishaji kwa jamii, pamoja na kuhakikisha huduma za uchunguzi zinapatikana kwa wakati.

Kwa upande wake, Dkt. Paul Shimba, Mkuu wa Kitengo cha Taarifa za Kimkakati wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma (NTLP), alisema Kikao kilihusisha OWM TAMISEMI, waratibu wa Kifua Kikuu, Ukoma na UKIMWI ngazi ya Mkoa na wilaya, Wadau watekelezaji, Wadau wa maendeleo, asasi za kiraia, na watoa huduma za afya.

Kikao hicho kilifanya tathmini ya utekelezaji wa programu kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2026, ambapo viashiria mbalimbali vya utoaji wa huduma za TB, UKIMWI na Ukoma vilipitiwa. Tathmini hiyo ilibaini kuwa utekelezaji ulifikia asilimia 82 ya malengo yaliyopangwa.

“Mafanikio yaliyopatikana yamewekewa mpango wa kuyaendeleza, huku changamoto zilizobainika zikiwekewa mikakati ya utatuzi ili kuongeza ufanisi na kufikia malengo ya kudhibiti na kutokomeza Kifua Kikuu na Ukoma nchini,” alisema Dkt. Shimba.

images-1.jpg


Naye Dkt. Allan Tarimo, Mkuu wa Kitengo cha Kinga na Matunzo ya TB na Ukoma wa NTLP, alisema kikao hicho kimeiwezesha Wizara kupata picha halisi ya utekelezaji wa afua za TB na Ukoma kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2026. Alisema matokeo hayo yatatumika kuimarisha utekelezaji katika nusu ya pili ya mwaka kwa lengo la kufikia asilimia 100 ya malengo yaliyowekwa ifikapo Desemba 2026.

Dkt. Tarimo, kwa niaba ya Meneja wa Mpango, alizishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI kwa kusimamia utekelezaji wa afua katika ngazi za mikoa na wilaya, Serikali ya Marekani kupitia Ubalozi wake nchini, pamoja na wadau wote walioshiriki katika kikao hicho